Jeshi
la Polisi Zanzibar limewakamata watuhumiwa wengine watatu wakiwemo
Maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA kituo cha Bandari
Zanzibar kwa kuhusika na kashfa ya kupatikana kwa meno ya tembo yenye
thamani ya Mabilioni ya shilingi.
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa
Ali Mussa, amewataja Maafisa hao wa TRA waliokamatwa kuwa ni Omari Hamad
Ali(50) na Mohammed Hija(48) ambao wote wanafanyia kazi katika Bandari
ya Zanzibar na mtuhumiwa mwingine ni kibarua wa Mamlaka ya bandari
Zanzibar Haidar Ahmad Abdallah(54).
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunaifanya idadi ya watuhumiwa waliokamatwa hadi sasa kwa kuhusika na sakata hilo kufikia watano.
Kamishna Mussa amesema Watuhumiwa
wengine wawili ambao ni wafanyakazi wa Kampuni ya Uwakala wa Mizigo ya
Island Sea Food Limited, Mohammed Suleiman Mussa(45) na Juma Ali
Makame(34) wao walikamatwa siku ya tukio la kukamatwa kwa meno hayo ya
tembo kwenye Bandari ya Zanzibar.
Tayari watuhumiwa hao wamesafirishwa
kwenda Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano
zaidi.Pamoja na mambo mengine, kusafirishwa kwa watuhumiwa hao kwenda
Jijini Dar es Salaam, kunatokana na Zanzibar kutokuwa na Sheria maalumu
inayohusu wanyamapori.
Maafisa wa Idara ya Wanyamapori nchini,
leo wamekamilisha kazi ya kuhesabu na kulinganisha vipande 1,023 vya
meno ya tembo vilivyokamatwa jana kwenye Bandari ya Zanzibar na kubaini
idadi ya tembo waliouawa kuwa ni 305.
Meno hao yenye uzito wa kilo 2,915
yenye thamani ya Dolla 4,775,000 sawa na shilingi 7,480,125,000 za
Tanzania (Bil.7.4), yalikamatwa juzi yakiwa yamehifadhiwa katika magunia
98 na kuwekwa kwenye konteina moja la futi 40 lenye namba PCIU 857619/0
lillilokuwa tayari kupakiwa kwenye meli ya MV Kota Henning kupelekwa
nchini Ufilipino kwa magendo.
Hadi sasa bado Makachero wa Polisi wa
Kimataifa Interpol hapa nchini kwa kushirikiana na Makachero wa Polisi
Zanzibar, idara ya wanyamapori makao makuu wanaendelea na upelelezi wa
kuwabaini wale tote waliohusika na kashfa hiyo.
Jana Kamishna wa Polisi Zanzibar CP
Mussa Ali Mussa, alisema kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kuhakikisha kuwa
upelelezi wa kina unafanyika ili kuwakamata wale wote wanaohusika na
mtandao huo.
Alisema hadi sasa Jeshi la Polisi bado
linamsaka tajiri aliyewezesha mipango ya kukusanywa na kusafirisha
shehena hiyo kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar ili kusafirishwa nje ya
nchi.
Aucun commentaire